Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, ikinukuu baadhi ya vyombo vya habari vya Uswisi, chama kimoja cha Kiislamu kinachomilikiwa na Waislamu wa Albania kilikuwa na nia ya kubadilisha jengo lililopo katikati ya kijiji cha “Siebnen” ndani ya kantoni ya Schwyz nchini Uswisi kuwa msikiti na kituo cha kitamaduni. Hatua hii ilikumbana na mwitikio hasi kutoka kwa sehemu ya wakazi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hii, wapinzani wametangaza kuwa; hawaoni kuwa ni jambo linalofaa kujenga msikiti katikati ya kijiji, na wameeleza wasiwasi wao kuhusu athari zake za kijamii na kitamaduni. Kwa upande mwingine, viongozi wa chama hicho cha Kiislamu wamesisitiza kwamba; lengo lao ni kuunda nafasi kwa ajili ya ibada na shughuli za kitamaduni, na hawana nia ya kusababisha mvutano au migogoro katika jamii ya eneo hilo.
Rais wa chama hicho cha Kiislamu alisema katika kauli zake kuwa: “Hatuna nia ya kuigawa jamii, na tunapendelea kupata suluhisho ambalo halitasababisha mvutano wala migogoro.”
Hatimaye, viongozi wa chama hicho walitangaza kuwa mradi huo kwa sasa umesimamishwa, na wanaendelea kuchunguza chaguo legine kwa ajili ya kupata mahali panapofaa kwa shughuli za kidini na kitamaduni za Waislamu.
Ripoti zinaonesha kuwa; suala la kuanzishwa kwa vituo vya ibada vya Kiislamu katika baadhi ya maeneo ya Uswisi wakati mwingine hukumbana na hisia nyeti za kijamii na upinzani wa ndani, na jambo hili limekuwa mojawapo ya mada zinazojadiliwa katika ngazi ya jamii za maeneo husika.
Maoni yako